AALCO WALAANI MAPIGANO BAINA YA ISRAEL NA PALESTINA

Nchi Wanachama wa Taasisi ya Mashauriano ya Sheria za Asia na Afrika ( AALCO) kwa kauli moja wamelaani vikali vurugu zinazoendelea kati ya Palestina na Israel na kuzitaka nchi hizo mbili kutafuta suluhu kwa njia ya amani
Kauli hiyo dhidi ya machafuko yanayoendelea baina ya Israel na Palestina ni Baadhi ya maazimio yaliyofikiwa mwisho mwa Mkutano wa 61 AALCO uliokuwa ukifanyika katika Mji wa Bali nchini Indonesia.
Wanachama wa AALCO , wameazimia pamoja na mambo mengine, kuendelea kushirikiana katika kuboresha kazi za Tume ya Sheria za Kimataifa inayosimamiwa na AALCO.
Mkutano huo ambao ulikuwa wa wiki moja, pia umeazimia kuendelea kutoa ushirikiano kwa AALCO katika jitihada zake za kuwajengea uwezo wanasheria katika Sheria za Kimataifa hususani Sheria za Bahari na Sheria za kimataifa za Uwekezaji na Biashara.
Ujumbe wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Mkutano huo, uliongozwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Balozi Kennedy Gaston.
Pamoja na kuhudhuria na kushiriki vikao mbalimbali vya Mkutano huo, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali pia alipata fursa ya kubadilishana Mawazo na Viongozi mbalimbali waliohudhuria Mkutano akiwamo Waziri wa Sheria na Haki za Binadamu wa Indonesia Bw. Yasonna H. Laoly.
Waziri Laoly pia ni Rais wa Taasisi ya AALCO kwa mwaka 2023/2024.
Katika mazungumzo hayo Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amempongeza Waziri Laoly kwa namna alivyoongoza mkutano huo kwa ufanisi na akamuahidi ushirikiano wakati wa kipindi chote cha uongozi wake kwenye Taasisi hiyo.
Naye Waziri Yasonna Laoly alimpongeza Mhe. Balozi Gaston kwa kuteuliwa kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali huku akimtakia kila la kheri katika utekelezaji wa majukumu yake.
Mwisho
22/10/2023