MABARAZA YA WAFANYAKAZI NI CHOMBO MUHIMU MAHALI PA KAZI-WAZIRI NDUMBARO
MABARAZA YA WAFANYAKAZI NI CHOMBO MUHIMU MAHALI PA KAZI-WAZIRI NDUMBARO
Na Mwandishi wetu
April 22 mwaka huu, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dk. Damas Ndumbaro alikuwa mgeni rasmi katika Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Baraza hilo lilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa jengo la Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Jiijni Dodoma na Mwenyekiti wake akiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dk. Eliezer Feleshi.
Ajenda kuu ya baraza hilo ilikuwa ni kupokea na kujadili taarifa ya Mpango na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2022/2023 ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Waziri Ndumbaro katika hotuba yake ya ufunguzi wa baraza hilo, pamoja na kupongeza kwa uhai wa baraza la wafanyakazi katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, pia alipongeza kwa namna Menejimenti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutekeleza jukumu la kisheria la kuwashirikisha watumishi kwenye mipango ya uendeshaji wa Taasisi.
Anasema, hatua hiyo ni njema, kwa sababu kila palipo na watumishi wengi pana mawazo mengi na hivyo ushirikishwaji kuhusu mipango ya uendeshaji wa Ofisi kunasaidia kupata mawazo shirikishi yanayorahisisha uendeshaji na pia ni fursa ya kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi.
“Katika vikao hivi ( Baraza La Wafanyakazi) ndiko tunapopata ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili watumishi, lakini pia watumishi wanapata morali ya kazi kama wanashikiri katika kuandaa na utekelezaji wa mipango ya Taasisi”. Amesema Waziri na kuongeza
“Hivyo, pamoja na kuwapongeza kwa hatua hii, ninatoa rai muendelee kufanya vikao kama hivi kama ilivyopangwa ili kudumisha pamoja na mambo mengine mahusiano mazuri baina ya Uongozi na Utumishi”. Akasisitiza Waziri wa Katiba na Sheria.
Akimkaribisha Waziri wa Katiba na Sheria kufungua Baraza hilo, Mwenyekiti wa Baraza Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe Jaji Dk. Eliezer Feleshi, aliwaeleza wajumbe wa Baraza kwamba, ukomo wa bajeti umeongezeka kutoka kiasi cha shilingi bilioni tano na milioni ishirini na mbili, mia tisa themanini na moja elfu ( Tshs 5,022,981,000) zilizotengwa mwaka wa fedha 2022/2023 hadi kufikia ukomo wa kiasi cha shilingi bilioni sita na milioni mia tisa ishirini na nne mia tisa kuma na nane elfu ( Tshs. 6,924.918,000/=) kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Kwa mujibu wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ongezeko hilo ni wazi linalenga kuiongezea uwezo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika utekelezaji wa majukumu yake kwenye mipango iliyopangwa kutekelezwa katika mwaka ujao wa fedha.
“Natoa rai kwa watumishi wote wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuongeza ubunifu na mikakati kabambe ili kutekeleza kazi za Ofisi kwa weledi wa hali ya juu” amesisitiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Baadhi ya wajumbe wa Baraza waliopata fursa ya kuchangia wasilisho la taarifa ya Mpango na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2022/2023 ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, walielezea kuridhishwa kwao na namna ambavyo wamekuwa wakishirikishwa na kushiriki hatua kwa hatua katika kuandaa bajeti hiyo.