Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI AAPISHWA KUWA KAMISHNA WA TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA
service image

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza Johari tarehe 7 Septemba 2024 ameapishwa kuwa Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, hafla hiyo fupi ya uapisho imefanyika katika ukumbi mdogo wa Bunge, Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Johari ameapishwa kutimiza takwa la Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Na. 4 Sura ya 237 inayomtaka kila Kamishna kuapishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali anachukua nafasi hiyo baada ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa.

Akizungumza mara baada ya kuapishwa kuwa Kamishna wa Tume ya Mahakama Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameahidi kutoa ushirikiano mkubwa kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya Tume hiyo. 

“Napenda kuchukua nafasi kuwaahidi kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu itachukua nafasi yake stahiki na kutoa mchango wake ipasavyo katika shughuli za Tume, kuhakikisha kwamba tunakuwa daraja zuri kwa Mihimili ya nchi katika kutekeleza majukumu yake”.

Katika hatua nyingine aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamishna ya Tume ya Utumishi wa Mahakama aliyemaliza muda wake Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mhe. Dkt Eliezer Mbuki Feleshi amemuomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kushirikiana na Tume hiyo katika kuhakikisha kuwa masuala mbalimbali ya Tume hiyo yanatekelezwa kwa ufanisi.

Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma, amemtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kutoa ushirikiano kwa kushiriki kwenye masuala mbalimbali yanayotekelezwa kwenye Tume hiyo. 

“Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni kiungo muhimu katika kuunganisha Mihimili ya nchi, hivyo sisi kwa upande wetu wa Mahakama tunamtegemea sana Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kutuwakilisha na kutusemea kwenye masuala mbalimbali yanayohusu Mahakama”.

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi

11 Sep, 2024
Maoni