Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali
NITAKUWA TAYARI KWENDA MAHAKAMANI -AG FELESHI
service image

NITAKUWA TAYARI KWENDA MAHAKAMANI –AG FELESHI

Na  Mwandishi Maalum

Dodoma

Mwanasheria Mkuu wa Serikali  Mhe.  Jaji  Eliezer  Feleshi ( AG) amesema  akiwa ni  Wakili wa Serikali namba moja yupo tayari kwenda mahakamani kuendesha mashtaka ya  jinai ikiwa itamlazimu kufanya hivyo.

AG Feleshi amebainisha hayo mwisho mwa wiki  katika   Mkutano wa  Baraza la Wafanyakazi la  Ofisi ya  Mwanasheria Mkuu wa Serikali  lililofanyika  katika Ukumbi wa Mikutano wa Jengo la  Zimamoto na Uokoaji  Jijini Dodoma. Mgeni   Rasmi katika    Baraza hilo alikuwa ni  Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dk. Damas Ndumbaro (Mb)

Utayari  wa Mwanasheria Mkuu wa  Serikali  kwenda  mahakamani  unatokana na matangazo  ya Serikali (GN)   namba 55, namba 56 na namba 97  yaliyotolewa  kwa nyakati  tofauti na  Mkuruganzi wa Mashtaka  Bw. Sylvestar Mwakitalu ambaye kupitia matangazo hayo amewateua na kuwatangaza mawakili wa serikali  168 akiwamo  Mwanasheria Mkuu wa Serikali  kuwa waendesha mashtaka ya jinai na watatekeleza  jukumu hilo kwa  maelekezo ya DPP.

”Mhe Waziri,  mwanzoni mwa mwaka huu,  Mkurugenzi wa Mashtaka aliteua na kuwatangaza  mawakili  168 na  kuwapatia ’intrustment’ ya  kuwa waendesha mashtaka  ya  jinai, na mimi kama  wakili namba moja jina langu lipo, kwa hiyo nitakuwa tayari kwenda mahakamani kama mwendesha mashtaka kama nitahitajika na kwa maelekezo ya DPP. Lakini pia nitumie nafasi hii kuwakumbusha mawakili wote  wateule  kwamba, instrument waliyopewa  siyo kitambaa cha mfukoni, wanatakiwa kuifanyia kazi na nitataka kuona  matokeo yake mwishoni mwa mwaka” akasisitiza   AG Feleshi

Aidha  AG Feleshi ambaye  katika nafazi zake za uongozi  amewahi pia kushika nyadhifa mbalimbali  zikiwamo  za  Mkurugenzi wa Mashtaka na Jaji, amewasisitiza maafisa Masuuli wa  Ofisi ya  Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Wizara ya Katiba na Sheria     kuweka mipango mikakati ya kuwezesha mawakili wateule kuendesha mashauri hayo kwa maelekezo ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

AG Feleshi amesema   uamuzi huo wa kuwateua na kuwatangaza  Mawakili wa Serikali kutoka  Ofisi  hizo    kuwa waendesha  mashtaka,  ni hatua  ambazo zimechukuliwa pamoja na mambo mengine,  zinalenga  katika kuharakisha uendeshaji  wa mashauri  mahakamani, kuongeza tija Serikalini na pia kuongeza ujuzi, uwezo na uzoefu wa Mawakili  waliopo katika Ofisi utumishi wa umma .

Aidha  kufuatia uteuzi huo  wa Mawakili wa Serikali 168  kuwa waendesha  mashtaka,  Mwanasheria Mkuu wa Serikali  amesema  hatarajii kuona  kuna mlundikano wa mashauri mahakamani au ucheleweshaji  kwa kile alichosema,  Ofisi ya Taifa ya Mashtaka  imeongezewa nguvu kazi.

AG Feleleshi  ameongeza kwamba, kupitia maboresho yanayoendelea  hivi sasa  yakiwamo ya kuwasajili   wanasheria  na  mawakili  wa serikali walipo katika utumishi wa umma kupitia  mfumo wa OAG-MIS, muda si mrefu utaratibu utawekwa kuhusu namna ya kuwatumia kikamilifu wanasheria wote walio katika ofisi za umma.

Katika hatua nyingine  Mwanasheria Mkuu wa Serikali  ameelezea  matarajio yake kwamba,   Wakili Mkuu wa Serikali  naye atatoa  Hati kwa Maafisa Sheria na Mawakili wa Serikali  itakayowezesha  kuendesha Mashauri ya Madai Mahakamani.

Akifungua   Baraza hilo,  Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dk. Damas Ndumbaro ( Mb) pamoja na kuipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa na Baraza la Wafanyakazi  lililo hai na linalofanya vikao vyake kwa mujibu wa sheria amewataka  Watumishi wa Ofisi  hiyo kutambua kwamba  wao ni  taswira ya Taifa kwenye masuala ya  Utawala na Sheria na akatoa rai   ya kuwataka kuendelea kutekeleza majukumu   hayo kwa weledi na uadilifu wa kiwango cha juu  na kwa mashalhi mapama ya Taifa.

Aidha Waziri Ndumbalo amesisitiza masuala kadhaa ambayo  watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  wanapaswa kuyazingatia katika utekelezaji wa majukumu yao,

Masuala hayo ni  pamoja na kufahamu vipaumbele ya serikali  na namna ya  kuoanisha vipaumbele  hivyo na  mipango ya  Ofisi ,  watumishi kuzingatia  Sheria, Kanuni na  miongozo ya Utumishi wa Umma  ili kuongeza tija na ubora wa kazi na kuwa waadilifu.

Ajenda  kuu iliyojadiliwa katika  Baraza hilo  ilikuwa ni  kupokea na  kujadili taarifa ya Mpango na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2022/2023 ya Ofisi ya Mwanasheria  Mkuu wa Serikali.

Imetolewa na  Kitengo  cha Mawasiliano

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali

25/4/2022

 

27 Apr, 2022
Maoni