AG FELESHI AELEZA MANUFAA YA MAWAKILI WA SERIKALI KUJISAJILI KATIKA MFUMO WA OAG-MIS
AG FELESHI AELEZEA MANUFAA YA MAWAKILI WA SERIKALI KUJISAJILI
Na Mwandishi Maalum
Dodoma
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Jaji Dk. Eliezer Feleshi amesema, usajiri wa mawakili wa serikali katika mfumo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali unaojulikana kama OAG-MIS ni zoezi endelevu na hivyo kuwataka wale ambao bado hawajajisajili kuendelea kufanya hivyo.
Akizugumza hivi karibuni mbele ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dk. Damas Ndumbalo (Mb) AG Feleshi amesema usajili wa mawakili hao wa serikali walio katika utumishi wa umma, unalenga pamoja na mambo mengine kuwatambu wapi walipo na wanafanya nini
Amesema, zoezi hilo na ambalo hakudhani kwamba lingekuwa gumu hasa kutokana na kwamba bado kuna mawakili wengi wanasuasua kujisajili katika mfumo huo.
Hadi kufikia tarehe 27April jumla ya mawakili wa serikali 1943 walikuwa wamejisajili kwenye mfumo huo na kati ya hao ni 1100 tu ndiyo waliokuwa wamejaza taarifa zao kwa ukamilifu.
Pamoja na kuwatambua lakini pia ni zoezi ambalo litaiwezesha Ofisi yake kutambua Mawakili hao wanatekeleza majukumu gani, ukubwa wa majukumu au uchache wa majukumu,sifa na uwezo wao.
AG Feleshi amebainisha kwamba, usajili huo pia utasaidia sana kuangalia namna bora ya kuwatumia mawakili hao katika maeneo mbalimbali kulingana na sifa na uhitaji, lakini pia kuwaongezea majukumu kwa wale ambao majukumu yao ni machache
Vile vile usajili huo utawawezesha Mawakili hao walio katika utumishi wa umma kutambuliwa na mamlaka mbalimbali ikiwamo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mahakama na kuorodheshwa kwenye Gazeti la Serikali.
Aidha upatikanaji wa takwimu za Mawakili hao kutaiwezesha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kujua namna ya kuboresha huduma za Sheria hapa nchini ili kuendana na wakati na mabadiliko yanayoendelea nchini na duniani kote.
Mwanasheria Mkuu ametoa rai kwa mawakili hao wa serikali katika utumishi wa umaa kuacha kuwa nyuma nyuma katika masuala na mambo yanayowahusu. Na kwamba kwa wale ambao watashindwa kujisajili bila ya kuwa na sababu za msingi watakosa kutambulika, watakuwa wamekiuka sheria na watachukuliwa hatua.