AG FELESHI AHAIDI KUSIMAMIA MAELEKEZO YA SERIKALI

Na Mwandishi Maalum
Kutoka Viwanja vya Chinangali
Dodoma
Mwanasheria Mkuu wa Serikalil Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi amemhakikishia Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba, ataendelea kusimamia kwa karibu maelekezo aliyotoa tarehe 29 Septemba 2022 ambayo yalitokana na maelekezo ya awali ambayo yeye Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyatoa kwa Watendaji wa Serikali.
Maelekezo hayo ni ya kuwataka Watendaji Wakuu wa Serikali pamoja na mambo mengine kutoa kipaumbele cha kumaliza migogoro kwa njia ya usuluhishi. Aidha Rais Samia Suluhu Hassani aliwataka septemba 29 2022 akizindua Chama cha Mawakili wa Serikali pamoja na mambo mengine aliwataka Mawakili wa Serikali kuhakikisha wanakuwa makini kusikiliza migogoro na kuhakikisha inatatuliwa kabla ya kufikishwa mahakamani.
Mhe. Feleshi amesisitiza kuwa Ofisi yake (OMMS) na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OSG) pia zitaendelea kutekeleza maelekezo ya kusimamia kwa niaba ya serikali matakwa ya kisheria ya kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi.
Mwanasheria Mkuu Feleshi ametoa ahadi hiyo leo Jumatano wakati alipokuwa akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Shera Nchini ambapo Mhe. Rais alikuwa mgeni rasmi. Maadhimisho hayo yamefanyika katika viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi wa mahakama, serikali, bunge, mawakili, wanafunzi na wananchi.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyezungumza katika hadhara hiyo muda mfupi mara baada ya Rais wa Chama cha Mawakili wa Kujitegemea ( TLS) Profesa Edward Hosea , amesema , pamoja na kutekeleza maelekezo aliyoyatoa Mhe Rais pia ataendelea kusimamia maelekezo aliyoyatoa kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali mnamo March 30,2022 kwa Watendaji Wakuu Serikalini la kuwataka pamoja na mambo mengine kutoa kipaumbelea cha kumaliza migogoro kwa njia ya maridhiano.
Mhe. Feleshi amebainisha pia kwamba, maelekezo yake hayo pia aliyapeleka kwa Mhe. Katibu Mkuu Kiongozi ambaye naye aliwasisitiza watendaji wa serikali kuwa hatua ya uvunjaji wa mikataba iwe ni suluhisho la mwisho baada ya njia zote za majadiliano kushindikana na kwamba uvunjaji huo ufanyike kwa kibali cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Pamoja na kusisitiza kuwa atasimamia maelekezo ya Mhe. Rais na yale ambayo yeye aliyatoa kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Mhe. Jaji Dkt, Eliezer Feleshi akatumia hadhara hiyo kuwakumbusha watendaji wa Serikali kuzingatia maelekezo hayo muhimu
Ili kuiishi kwa vitendo kauli mbiu ya siku ya sheria nchini kwa mwaka 2023. Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa rai kwa waheshimiwa Majaji na Mahakimu kuwa tayari kuwasilisha Ofisini kwake kupitia dawati linaloshughulika na utendaji kazi wa Mawakili wa Serikali kuhusu wakili yeyote wa Serikali ambaye kwa namna yoyote atathibitika kudhoofisha jitihada za Serikali na Mahakama za kutumia njia za usuluhishi katika kutatua migogoro.
Katika hatua nyingine Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema wakati umewadia wa kuboresha tena Sheria ya Mwenendo wa Madai, Sura ya 33 ili shauri la madai lipate sifa ya kusajiliwa mahakamani endapo kuna uthibitisho kwamba limepitia hatua zote za usuluhishi na ikashindikana.
Kwa upande wake Rais Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameagiza Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Fedha na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kushirikiana na kuzifanyia marekebisho sheria zenye mizunguko mingi na hivyo kuchelewesha utoaji wa haki.
Naye Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Profesa Ibrahim Juma amepongeza mapendekezo yaliyotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa kuzifanyia mabadiliko baadhi ya sheria zenye milolongo mirefu na kwamba marekebisho hayo yatasaia sana.
Vile vile Jaji Mkuu ametoa rai pia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhakikisha kuwa suala la usuluhishi wa migogoro nje ya mahakama liwe la lazima na jambo hilo limo ndani ya uwezo wake.
Kauli mbiu ya Siku ya Sheria nchini ilikuwa umuhimu wa utatuzi wa Migogoro kwa njia ya usuluhishi katika kukuza uchumi Endelevu: Wajibu wa Mahakama na Wadau”.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano
01/02/2022