Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali
AG FELESHI AISHUKURU ALSF KUWAJENGEA UWEZO WATAALAMU WA NDANI
service image

Na Mwandishi Wetu

Dodoma

12 SEPTEMBA 2022

Mwanasheria  Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dk. Eliezer Feleshi amesema  mataifa mengi  ya Afrika yamekuwa yakipoteza kesi  nyingi   katika mahakama za kimtaifa na  mabaraza ya usuluhishi  kutokana  Mawakili wao kutokuwa na umahiri wa kutosha  unaoendana na  kasi ya mabadiliko  ya kiuchumi na kimaendeleo.

Na kwa sababu hiyo amesisitiza haja na umuhimu kwa mawakili hao wa Serikali pamoja na wataalamu wengine wakiwamo  wachumi na manunuzi kujengewa uwezo na umahili   na ubobevu wa kuweza kukabiliana na changamoto za dunia ya sasa.

Ameyasema hayo wakati alipokutana na kufanya  mazungumzo na  Bi. Aida Sylla na Bi. Manuela Dieng  ambazo ni wataalamu kutoka Taasisi ya Kimataifa ya The African Legal Support Facitility ( ALSF)  Mazungumzo hayo yamefanyika  Katika  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu iliyopo  katika Jengo la Bunge  Dodoma.

ALSF ipo chini  ya Banki ya Maendeleo ya Afrika ( AfDB) yenye Makao yake Makuu Abidjani, Cote d’Ivoire. Na inato pamoja na  mambo mengine ushauri  wa kisheria katika  nchi za Afrika pamoja na  mafunzo ya  kuwajengea uwezo wataalamu katika nchi hizo.

Wataalamu hao wapo  Mkoani Dodoma kwaajili ya  mafunzo  mafupi ya kuwajengea uwezo , umahili   na  ujuzi  adimu  wataalamu wakiwamo  mawakili wa serikali katika  maeneo mbalimbali ya  uwekezaji mkubwa ikiwamo eneo la  uchimbaji madini. 

“Wataalamu  wetu hapa  Tanzania na Afrika kwa ujumla  wakiwamo   wanasheria, wachumi na watu wa manunuzi  wanakabiliwa na  changamoto nyingi,tunahitaji  kuwajengea uwezo na  umahili  wa mara kwa mara, Afrika  tunapoteza kesi nyingi kwasababu  tunapungukiwa  ujuzi na utaalamu wa kiwango cha kimataifa, nipende kutoka  shukrani zangu za dhati kabisa kwa  ALSF  kukubali ombi la Ofisi yangu  la kuja kutoa mafunzo  huu ni mwanzo mzuri wa ushirikiano endelevu” akabainisha  Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Aidha amesema, amefurahishwa pia kwamba miongoni mwa wataalamu  watakao shiriki mafunzo hayo  wapo kutoka  Tanzania Visiwani kwa kile alichosema yapo masuala mtambuka yanayohusu pande mbili za Muungano  ambayo wataalamu wake wanapaswa kuwa na uelewa wa pamoja.

Naye Bi  Manuela Dieng akizungumza kwa niaba ya mwenzake,  amesema   ALSF imefurahi kuja kutoa mafunzo  hayo na kwamba huo ni mwanzo na akamwomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali  Eliezer Feleshi kuainisha maeneo  zaidi  ambayo  anadhani  yanahitaji kujengewa uwezo.

Vile vile wameelezea kuridhishwa kwao na ushirikiano ambao wanaupata  kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar na kwamba wanaendelea  pia na majadiliano ya maeneo zaidi ya kuwajengea uwezo.

 Baadhi ya Taasisi na  Wizara zinazoshiriki mafunzo hayo ni    Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali,  Bunge, EWURA, PURA, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Nishati, Wizara ya Madini, Kamisheni ya Madini   Ofisi ya  Mwanasheria Mkuu  Zanzibar.

12 Sep, 2022
Maoni