Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali
AG FELESHI ASISITIZA HAJA NA UMUHIMU WA OFISI YAKE KUNDELEA KUPATA HATI  SAFI
service image

 

Na Mwandishi Maalum

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer   Feleshi  amemtaka  Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikaki  Mhe. Balozi Prof. Kennedy Gaston  kuhakikisha Ofisi  ya  Mwanasheria  Mkuu wa Serikali, inaendelea  kupata    hati safi ya ukaguzi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikalia ( CAG)

Amesisitiza kuwa  jambo hilo la Ofisi  kuendelea kuwa na hati safi linaweza likawa la kushangaza  lakini  ni  jambo la msingi  na muhimu sana kwa Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali  jambo ambalo  linakwenda sambamba na  usafi na maadili ya Ofisi.

Ameyasema hayo siku ya  jumatano( septemba  20,2023) wakati wa hafla ya kumkaribisha rasmi  na kukabidhiwa  Ofisi  Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Balozi Prof. Kennedy  Gaston, hafla hiyo, iliyofanyika katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu  wa Serikali  Mtumba Jijini Dodoma, pia  ilihusisha kumuaga aliyekuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali  Dkt. Evaristo Longopa ambaye sasa ni Jaji wa Mahakama Kuu.

  Dkt. Evaristo Longopa aliyekuwa  Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, alimkabidhi  Naibu  Mwanasheria Mkuu wa Serikali   Balozi Prof. Kennedy Gaston   Ofisi ya Naibu  Mwanasheria Mkuu wa Serikali Pamoja na  Nyaraka mbalimbali muhimu  zinazosimamia utekelezaji wa  Majukumu  yake

Mhe. Feleshi  amebainisha  kuwa katika  kipindi chote cha takribani miaka mitano ambayo Dkt. Longopa aliyotumikia kama Naibu  Mwanasheria Mkuu wa Serikali yapo mambo mengi ambayo ameyatekeleza na kuyasimamia kwa karibu sana.

“Tunamshukuru sana  Dkt.Longopa, kati ya  vitu hata nikisahau, yeye na timu yake ya  manejiment, anaondoka tukiwa na hati safi kutoka kwa  Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, unaweza ukashangaa , lakini hili ni eneo muhimu sana kulilinda ( hati safi)  pamoja na  maadili na usafi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu  wa Serikali) akasisitiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali  Jaji Feleshi.

Aidha  Pamoja  na  kumtaka  Naibu Mwanasheria Mkuu Gaston kuhakikisha Ofisi inaendelea kupata hati safi, pia amemtaka  Pamoja  na mambo mengine ya  kiutendaji yanayomhusu  kama  Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni   kuhakikisha kwamba Nakala za Mikataba ambazo  zimekwisha sainiwa  na  wizara na Taasisi baada ya kufanyiwa upekuzi zinarudishwa  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Nakuona unakazi nyingi kuliko mimi,  kwa sababu watu au wadau wetu watakaoshindwa kunipata mimi kwa sababu yoyote ile watakuja kwao si semi kwamba utafanya kazi kwa saa 24 lakini  hili linaweza kutokea kwa mazingira ya  Ofisi yetu” akabinisha

Akasisitiza kuwa  ni muhimu Ofisi kuwa na nakala ya mkataba au mikataba iliyosainiwa  ili kuiwezesha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufuatilia.

 Katika  hatua nyingine   Jaji Feleshi amemtaka pia Naibu Mwanasheria Mkuu wa  Serikali  Prof Gaston  kuendeleza  juhudi za  kuboresha  hali bora ya watumishi,  matumizi ya mifumo ya tehama huku akiwataka  watumishi wote wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kumpatia  ushirikiano Naibu Mwanasheria Mkuu  Pamoja na kudumisha upendo, mshikamano na umoja  na  kuombeana.

Kwa upande wake Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali   Mhe.  Balozi Prof. Kennedy Gaston  ameshukuru  kwa mapokezi  mazuri na ukarimu alioonyeshwa na watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  na kwamba anashukuru kuwa sehemu ya familia ya Ofisi ya Mwanasheria  Mkuu wa Serikali.

Amewashukuru  watumishi wote kwa kuahidi kumpatia ushirikiano, huku  akiwataka kutokuwa na  hofu wala uoga na kwamba  jambo la msingi ni kazi iendelee.

Akizungumza kwa  niaba ya  watumishi wote,  Bi. Esther Cheyo  Katibu Sheria  Mkuu,  alimuhakikishia ushirikiano  wa watumishi wote katika utekelezaji wa majukumu yake.

Kwa upande wake Mwandishi Mkuu wa Sheria,  Bw. Onorius Njole akizungumza kwa niaba ya  Menejiment amesema  Menejimenti itampatia ushirikiano na  kuahidi kufanya  naye kazi kwa karibu kama ilivyokuwa  kwa mtangulizi wake.

Naye  Jaji wa Mahakama Kuu  Mhe. Dkt. Evaristo Longopa Pamoja na kutoa shukrani zake kwa  ushirikiano  ambao watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu  walimpatia katika kupindi  chote alichofanya kazi  nao, amewahimiza watumishi hao kuendelea kuchapa  kazi kwa bidii, maarifa na kujituma.

mwisho

21 Sep, 2023
Maoni