AG FELESHI ATAKA WANANCHI WASIZUNGUSHWE

Na Mwandishi wetu
Nyerere Square
22/1/2022
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe, Jaji Dkt. Eliezer Feleshi amewataka Mawakili wa Serikali wanaotoa huduma katika wiki la utoaji elimu na maonyesho ya Sheria ambayo yameanza leo ( Jumapili) katika Viwanja vya Nyerere Jijini Dodoma, kutowazungusha wananchi wanaokwenda kupata ushauri na msaada wa Kisheria.
Ametoa maelekezo hayo wakati alipokuwa akizungumza na Mawakili wa Serikali wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wanaotoa huduma katika Banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Viwanja hivyo vya Nyerere.
“Nisingependa kuona au kusikia mwananchi anazungushwa, akija mteja hapa na shida yake lakini mkagundua kwamba shida yake inapaswa kushughulikiwa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka au Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali basi mmoja wenu ainuke akamchukue Wakili wa Ofisi husika aje hapa badala ya kumzungusha mteja”
Amebainisha kwa kusema hatua hiyo inapashwa pia kuchukuliwa na Ofisi ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu kwa kubadilishana wateja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali badala ya kuwazungusha ningependa ushirikiano huu muwe nao katika Taasisi zote.
Vile vile Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema asingependa kupata aibu ya kukosekana kwa wakili wa Serikali katika Banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
“Sitaki aibu, wakati wote muwepo katika banda ili mtoe huduma kwa wananchi watakaokuja, haitapendeza mwananchi hanafika hapa na hakuna mtu” amesisitiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametembelea banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mabanda ya Taasisi nyingine.
Kabla ya kutembelea Mabada nayo Mwanasheria Mkuu wa Serikali alikuwa mmoja wa Viongozi walioshirikia maandamano yaliyoanzia katika Jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma na kumalizikia katika Viwanja vya Nyerere.
Maadhimisho ya Siku ya Sheria yamezinduliwa leo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Isidori Mpango na Kilele Chake ni Februri Mosi,2022 katika Uwanja wa Chinan’gali jijini Dodoma na Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kauli mbiu ya Maadhimisho hayo ni “ umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia ya Usuluhishi katika kukuza Uchumi Endelevu Wajibu wa Mahakama na Wadau.
Banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali linahudumiwa na Mawakili wa Serikali kutoka Divisheni ya Mikataba, Divisheni ya Uratibu na Ushauri wa Kisheria na Divisheni ya Uandishi wa Sheria na maafisa wa kada nyingine.
mwisho