AG FELESHI AWAPA SOMO MAWAKILI WA SERIKALI WAPYA

Na Mwandishi Maalum
DODOMA
10/08/2022
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dk. Eliezer Feleshi ameelezea nia na adhama yake ya kurejesha heshima ya Mawakili wa Serikali.
Ameonyesha nia hiyo leo ( Jumatano) wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mawakili wa Serikali 48 ambao wameajiriwa hivi karibuni.
Katika mazungumzo hayo na ambayo pia yalihudhuriwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ( DPP) Bw. Sylvesta Mwakitalu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema anatarajia kuirejesha heshima kwa Mawakili wa Serikali kama ilivyokuwa miaka kadhaa ya nyuma,
“Tuliona tukutane nanyi ili tuweze kufahamiana, kuelezana masuala ya awali kabla hamjaendea kwenye Vituo vyenu vya kazi. Lakini ninataka mtambue ukubwa wa dhamana na heshima tuliyowapa ya kuwa Mawakili wa Serikali. Kubwa kwenu ni kutambua nyinyi sasa ni Mawakili wa Serikali” Akasitiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Akawaeleza Mawakili hao ambao ajira yao imezingatia uwiano wa jinsia kuwa “ Miaka kadhaa iliyopita, tulikuwa tunasema, sisi ni zaidi ya Bunge, ni zaidi ya Mahakama siyo kwa bahati mbaya ni kutokana na majukumu yetu na mfumo wa utekelezaji wa majukumu yetu, ningependa kuirudisha heshima hiyo kuanzia kwenu hasa kutokana na mchujo mkubwa tulioufanya mpaka kuwapata”.
Akizungumzia namna Mawakili hao walivyopatikana. Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa zaidi ya watu 1000 waliomba nafasi ya kuajiriwa. Baada ya mchujo mkali walipatikana watu 272 ambao nao walichujwa hadi kupatikana Mawakili hao 48.
Mwanasheria Mkuu amewataka Mawakili hao ambao kabla ya kuajiriwa Serikali walikuwa ni mawakili wa kujitegemea , kuwa sasa wanatakiwa kujitofautia na Mawakili wa kujitegemea.
Amewatahadharisha Mawakili hao kujiepusha na vitendo vitakavyokwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma, vikiwemo vitendo ya rushwa.
“Niwaombe sana mkazingatie maadili ya utumishi wa umma. Hivi itakuwaje baada ya muda nipate taarifa kuwa miongoni mwenu kuna waliochukua rushwa, jiepusheni na vitendo kama hivyo mkatende haki, nafahamu kuna vishawishi vingi, lakini ukikumbana na hali kama hiyo sisi viongozi wenu milango ipo wazi njooni kwa ushauri”.
Pamoja na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na dhamana waliopewa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesisitiza pia suala na unadhifu kwa Mawakili wa Serikali kuwa ni jambo ambalo ni lazima na si la hiari.
Akawataka kujijengea utamaduni wa kujiendelea wakiwa kazini, kuwa wabunifu na wanaopeda kujifunza na kuonya Wakili yeyote ambaye atapuuzia suala la kujiendeleza na kujiongezea maarifa atakuwa ni aduni mkubwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakilitalu amewaeleza Mawakili hao kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ni Ofisi kubwa, nyeti na zenye majukumu makubwa kwa Taifa .
“Majukumu ambayo sasa mnakwenda kuyafanya ni majukumu nyeti na makubwa. Mtafanya maamuzi ya kushtaki au kutoshtaki. Maamuzi hayo ukiyakosea kuna haki ya mtu itapotea na kuna muathirika hata pata haki yake”. Akatahadharisha DPP.
“ Katika utekelezaji wa majukumu yenu, mtatoa ushauri, ushauri wako unaweza kuliingiza taifa kwenye hasara na shida kubwa, kwa hiyo mnaweza kuona ukubwa wa majukumu yenu, wengi hapa mmetoka kwenye kampuni binafsi za uwakili tunatarajia mtafanya kazi zenu kwa weledi, kwa uaminifu na kwa kuzingatia miiko ya sheria,”
Aidha amewataka mawakili hao kutambua kwamba sasa wao ni maafisa wa mahakama kwa sababu hiyo wanatakiwa kuisaidia mahakama katika kutenda haki kwa mujibu wa sheria na kuachana na ujanja janja.
Mawakili hao pia walikula kiapo cha ahadi ya Uadililfu kwa Utumishi wa Umma zoezi liloendeshwa na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Joseph Pande. Viongozi wengine waliohudhuria mazungumzo hayo ni pamoja na Kaimu Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Onorius Njole na WSakurugenzi wa Utawala na Raslimali watu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.