CHAMA CHA MAWAKILI WA SERIKALI NA CHAMA CHA MAWAKILI TANGANYIKA KUSHIRIKIANA

Na Mwandishi Wetu
Mtumba-Dododma
Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika ( TLS) Profesa Edward Hosea amesema Chama chake kipo tayari kushirikiana na kufanya kazi kwa karibu na Chama cha Mawakili wa Serikali (TPBA).
Ameeleza nia hiyo jana alhamisi (Desemba 22,2022) wakati alipokutana na kuwa na mazungumzo na Uongozi wa Mpito wa Chama cha Mawakili wa Serikali ( TPBA) uliokwenda kujitambulisha kwa Uongozi wa TLS .
Profesa Hosea amelitaja eneo ambalo TLS na TPBA wanaweza kushirikiana kama likiwekewa mpango mkakati mzuri ni eneo la utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi.
Akiongea na mwandishi wa Habari hii, Katibu wa TPBA Bi. Sia Mrema amesema Rais huyo wa TLS pamoja na kushukuru kwa Uongozi wa TPBA kuona haja na umuhimu wa Kwenda kujitambulisha kwa uongozi wa TLS pia alionyesha nia ya wazi kabisa ya vyama hivyo kushirikiana kati baadhi ya maeneo ambayo vyama hivyo vinashabihiana likiwemo hilo la utoaji wa msaada wa kisheria kwa wananchi.
Bi. Mrema amesema TPBA imeona na kukubaliana juu ya wazo hilo la kushirikiana katika utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria ingawa kimsingi Wizara ya Katiba na Sheria ndiyo inayosimamia huduma hiyo lakini Vyama hivyo vina idadi kubwa ya Mawakili licha ya kuwa vinatekeleza majukumu yao katika mazingira tofauti.
Katibu huyo wa TPBA alibainisha Zaidi kwakusema, “Tumekwenda kujitambulisha kwa wenzetu na tumepokelewa vizuri sana na kwa kweli wao wamefarijika kwa sisi Kwenda kujitambulisha na sisi tumefarijika kwa namna tulivyopokewa lakini kubwa Zaidi kuwa na mazungumzo yenye tija”,
Akasema uongozi wa TPBA ulitumia ziara hiyo kuelezea kwa ufupi Taarifa ya TPBA na uwepo wake na nia ya kuwa na ushirikiano wa karibu na TLS katika baadhi ya maeneo. “Tulikuwa na majadiliano ya kina kueleza taarifa fupi ya Chama chetu na kwamba tupo , lakini pia kuona namna gani tunaweza kuwa na ushirikiano katika baadhi ya maeneo” akasema Bi. Mrema
Na kuongeza kuwa eneo moja wapo ambalo wamekubaliana kuliwekea mpango mkakati ni katika eneo la utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Bi. Sia Mrema eneo jingine ambalo wamekubaliana kuangalia namna ya kushirikiana ni katika eneo la uhuishaji wa taarifa za mawakili wa serikali katika Kanzi Data ya TLS inayofahamika kama Wakili Data Base pamoja na kubadilishana uzoefu katika maeneo mengine.
Kuhusu sjuala Uhuishaji wa taarifa za wanachama kutasaidia pamoja na pamoja na masuala mengine kutasaidia kufahamu wanachama walio hai hususani mawakili wa Serikali.
Vyama hivyo pia vimekubaliana kuona namna gani mifumo ya kanzi data ya OAG-MIS na Wakili Data Base itakavyoweza kusomana katika baadhi ya maeneo. Na kuongeza kuwa tayari wataalamu wa TEHAMA wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na TLS wameanza mawasiliano.
Katibu wa TPBA ameeleza pia kwamba waliwasilisha ombi kwa uongozi wa TLS la kuomba Mawakili wa Serikali ambao wapo katika orodha ya wanaodaiwa ada za TLS wasiondolewa katika kanzi data kwanza ili uongozi wa TPBA uone namna ya kulishughulikia tatizo hilo.
Wakijibu ombi hilo Uongozi wa TLS umeushauri uongozi wa TPBA kuandika barua rasmi kuhusiana na suala hilo.
Chama cha Mawakili wa Serikali kilizinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa Mkutano Mkuu Maalum wa Mawakili uliofanyika Septemba 29,2022 Jijini Dodoma.
mwisho