DAG GASTON AHAIDI USHIRIKIANO NA FURAHA KWA WATUMISHI WA OMMS

Na Mwandishi Maalumu
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Balozi, Prof. Kennedy Gaston ameahidi kumsaidia Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi kwa kutekeleza majukumu yake kwa ueledi.
Ametoa ahadi hiyo leo Alhamisi ( Septemba 14,2023) wakati alipowasili katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mkoani Dar Es Salaam muda mfupi mara baada ya kuapishwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Magogoni Jijini Dar es Salaam.
Alipowasili katika Ofisi ya MMS Mkoani Dar Es Salaam alipokelewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Feleshi, Mwandishi Mkuu wa Sheria Onerius Njole, Mkurugenzi wa Utawala na Raslimali Watu Silas Marwa , Wakili wa Serikali Mkuu Mwema Pumzi, Mawakili wa Serikali na watumishi wanaohudumu katika Ofisi ya Mkoa wa Dar es Salaam
Pamoja na kutoa ahadi hiyo ya kumsaidia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Balozi Prof, Gaston pia ameahidi ushirikiano, mshikamano na kuendeleza yale yote ambayo yamekuwa yakifanyika ikiwa ni Pamoja na kuendelea kuwajengea uwezo watumishi na kuwafanya watumishi wote wa OMMS kuwa watu wenye furaha.
“Kwanza nishukuru sana kwa mapokezi mazuri, niseme ,nimeheshimiwa sana kuwa mwanachama ya timu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, nikiwa mwanachama mpya ninaahidi kuwa mwanachama hai nitakayeendeleza kulizungusha gurudumu katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili Pamoja na mambo mengine kazi iendelee” akasema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuongeza
“Wataalamu wana msemo wao kwamba, chumba kisichojaa ni chumba ambacho kinahitaji maboresho hivyo nina amini kuwa bado ninayo nafasi kubwa ya kuchangia maboresho ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali”.
Akizungumza Zaidi katika hafla hiyo ya kumkaribisha, Balozi Gaston alimuahidi Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kusema, yeye kama Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali atakuwa wa kwanza kati ya walio sawa ( the first among the equals) na kwamba itakuwa timu itakayofanya kazi na kukaa Pamoja.
Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi akimkaribisha Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Pamoja na kumhakikishia ushirikiano wa hali ya juu alisisitiza kwa kusema yeye ( Mwanasheria Mkuu ) anapenda Ofisi yake iwe na watu wenye furaha lakini pia wachakapakazi.
“ Kanuni yangu ni 1+5 yaani kila Wakili wa Serikali Mwandamizi lazima awe na watu watano nyuma yake kwaajili ya kujenga timu imara, hii ndiyo kanuni yangu” akasisitiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Akizungumza kwa niaba ya Watumishi wa Ofisi ya MMS Mkoa wa Dar Es Salaam, Wakili wa Serikali Mkuu Mwema Pumzi alimuahidi ushirikiano wa hali ya juu Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika utekelezaji wa Majukumu yake.
Mwisho