Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali
HESHIMA YA MAWAKILI WA SERIKALI HAIWEZI KUSHUKA KAMA MANA- WAZIRI NDUMBALO
service image

   Na Mwandishi Maalum

3/11/2022

DODOMA

Waziri wa Katiba na  Sheria,  Dkt. Damas  Ndumbalo (Mb)  amesema,  heshima na hadhi ya  mawakili wa serikali haiwezi kushuka kama mana bali ni  kwa   uongozi   wa Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA))     kuhakikisha  heshima hiyo na hadhi vinarejea kwa    Mawakili wa Serikali nchini.

Ameyasema hayo   leo ( Alhamisi)  wakati  ujumbe wa  viongozi wa  Chama hicho   ukiongozwa na Rais wa Chama hicho Wakili Msomi Michael Marcellus Luena ulipokwenda Ofisini  kwake Mtumba, Jijini Dodoma kwa lengo la kujitambulisha.

Chama cha Mawakili wa Serikali  kilizinduliwa rasmi na Mhe. Samia Suluhu Hassan,  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Mkutano Mkuu wa Mawakili wa Serikai  uliofanyika Septemba 29 Jijini Dodoma

Baada ya  Mhe. Rais kuzindua   Chama hicho. Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi kwa mamlaka aliyonayo  aliteua  viongozi wa  mpito.

Viongozi walioteuliwa  ni  Wakili Msomi  Michael Marcellus Luena ambaye ni Rais,  Makamu  Rais ni  Wakili Msomi Lucas Charles Malunde,  Mwenyekiti ni Wakili Msomi Stephano Seba Mbutu, Makamu mwenyekiti  Wakili Msomi Hassan Mayunga, Katibu akiwa ni Wakili Msomi Sia Beatrice Mrema  na mweka  hazina Wakili Msomi Irene Joseph Luselie.

“Wanachama wenu wanataka kuona   wanathaminiwa na  wana hadhi , na hili  haliwezi kushuka kama mana, ni moja ya kujukumu lenu kama viongozi  pamoja na  mambo mengine, kuwafanya wajisikie hivyo”.  akasema Waziri  Ndumbalo

Katika  mazungumzo hayo na ambayo pia yalihudhuriwa na Katibu Mkuu   Mary Makondo, Waziri Ndumbalo  amebainisha  kuwa  katika nchi nyingine,  Wakili wa Serikali au  Mwanasheria wa Serikali  anaheshima sana na anahadhi ya  juu.

“ Kwa hiyo, mnakazi kubwa ya kufanya  branding  cha  chama chenu  lakini pia ya mawakili wa  Serikali, Chama lazima kionekane kipo na kinafanya kazi.”akasisitiza Waziri.

Akielezea zaidi kuhusu  kusafisha taswira ya  Mawakili wa Serikali, Waziri wa Katiba na Sheria alitolea mfano kwa kusema

 “ Jana ( jumatano) kulikuwa na mjadala mkali  Bungeni kuhusu mikataba, mpaka ikaonekana wanasheria ni wa ovyo, lakini wakati mwingine shida si wanasheria kwa hiyo mnayo kazi ya kusafisha taswira ya wanasheria wa Serikali”

Ameutaka  uongozi huo  kuhakikisha , Mawakili wa Serikali popote walipo  kutoruhusu  mkataba wowote kutumia  bila ya  kupita kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali  lakini pia kuhakikisha  wanashirikishwa na kuhusika  katika hatua zote zikiwamo  za majadiliano ya mkataba huo.

Waziri Ndumbalo  pia ameuagiza uongozi huo    kutetea maslahi na stahiki za wanachama wao.

“Unakuta wakili wa serikali  anasimama mahakamani kuitetea serikali  kwenye kesi zinazohusu  mabilioni ya fedha lakini  hali yake kwa maana stahili zake na maslahi yake ni suala jingine hivyo  mnaowajibu pia wa kulifanyia kazi hili la maslahi bora ya wanachama wenu.  

Katika hatua nyingine Waziri Ndumbalo  ameutaka uongozi huo  kuwa na mahusiano ya karibu  na Chama cha Mawakili Tanganyika ( TLS).

Vile vile amewataka viongozi hao  kujenga mazingira mazuri yatakayokiwezesha Chama cha Mawakili wa Serikali kushiriki  na kutoa mchango wao katika mijadala mbalimbali  inayohusu masuala  ya Sheria zikiwamo sheria zinazopelekwa  Bungeni.

Awali  Rais wa PBA Wakili Msomi Michael  Luena akielezea nia ya ziara hiyo,  alisema pamoja na kujitambulisha lakini pia wajumbe wameanza  vikao vyao vya awali vya ambapo wanajadili      masuala  mbalimbali  yanayohusu Chama hicho.

Viongozi hao  pia wameahidi kuyafanyia  masuala yaliyoainishwa na  Waziri Ndumbalo kwa mstakabali wa chama na wanachma.

Mwisho.

 

03 Nov, 2022
Maoni