JICA YAONYESHA NIA YA KUSHIRIKIANA NA OFISI YA MWANASHERIA MKUU

Na Mwandishi Maalumu
Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japani ( JICA) limeelezea nia yake ya kutaka kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika maeneo mbalimbali.
Nia hiyo ya JICA, imeelezwa leo ( Jumatatu )na Bw. Asano Siezaburo mwakilishi wa JICA Ofisi ya Tanzania, wakati walipokutana na kufanya mazungumzo na Kaimu Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Onorius Njole.Mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma.
“ Tumekuja tujadiliane na kuona ni maeneo gani Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inaweza kunufaika na misaada inayotolewa na JICA, hii ni kwa sababu tunataka kuwa na ushirikiano na Ofisi hii”. Akabainisha Bw. Seizaburo aliyekuwa ameambatana na Bi. Yukiko Karanuki katika mazungumzo hayo.
Moja ya eneo ambalo JICA imeonyesha nia ya kutaka kusaidia ni katika eneo la kujenga uwezo ( Capacity Building) kwa Mawakili wa Serikali.
Kwa kuanzia JICA itatoa fursa kwa Mawakili watatu (3 ) kwenda kujengewa uwezo kwa kuwapatia mafunzo katika eneo la Sheria za Biashara.
Ujumbe huo wa JICA umeitaka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuainisha maeneo mengine ya ushirikiano na kisha kuwasilisha JICA kwa majadiliano zaidi.
Kwa upande wake Kaimu Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Njole ameishukuru JICA kwa kuona umuhimu wa kutaka kuwa na ushirikiano na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Akasema , huduma za Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni mtambuka zinazogusa kila sekta ya nchi hii na kwa sababu hiyo nia hiyo ya JICA ya kutaka kuwa na mahusianao na OMMS ni muhimu sana.
“Karibu katika kila misaada ambayo JICA inatoa hapa Nchini iwe TANESCO kama ulivyosema, au katika Sekta yoyote ile, kuna mkono wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na hili halikwepeki kwa hiyo kila mnapotoa ushirikiano katika sekta fulani basi muikumbuke Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Mmefanya vema kuona umuhimu wa Taasisi hizi mbili kuwa na majadiliano ya kuona namna gani tunaweza kushirikiana”. Amesisitiza Bw. Onorius Njole ambeye pia ni Mwandishi Mkuu wa Sheria.
Aidha, Kaimu Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameishukuru JICA pia kwa kutoa fursa ya kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali katika eneo la Sheria za Biashara na kwamba mwanzo huo ni mzuri.
Akaahidi kwamba, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaangalia maeneo mengine ya ushirikinao
Katika mazungumo hayo, Kaimu Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliambatana na Bi.Slyvia Matiku, Mkurugenzi Msaidizi Divisheni ya Uratibu na Huduma za Kisheria na Bw. Sunday Hyera Mkurugenzi Msaidizi Divisheni ya Mikataba .
11/7/2022