KAMATI YA BUNGE YAPONGEZA MRADI WA KITUO JUMUISHI CHA TAASISI ZA KISHERIA ZA SERIKALI

Na Mwandishi Wetu
Busweru - Mwanza
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeupongeza mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Taasisi za Kisheria za Serikali na kuuelezea kuwa ni mradi wa mfano wa kuigwa.
Wametoa pongezi hizo leo Alhamisi wakati walipoutembelea mradi huo unaojengwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Kata ya Busweru Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya kupata maelezo ya mradi huo na kisha kuutembelea, Wabunge hao wametaka mradi huo ukamilike kwa wakati kama ilivyo kwenye mpango kazi.
Zaidi ya wabunge tisa (9) wa kamati hiyo waliuliza maswali mbalimbali kwa Mkandarasi (SUMA-JKT) na Mshauri elekezi (TBA) mengi ya maswali hayo yaliyoambatana na pongezi na yalitaka ufafanuzi kuhusu mradi.
Akizungumza mara baada ya wabunge hao tisa kupata fursa ya kuuliza maswali Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Florent Laurenti Kyombo (Mb) alimtaka Waziri wa Katiba na Sheria kuyafanyia kazi baadhi ya masuala yaliyoibuliwa na wabunge hao.
“Mhe. Waziri (Ndumbaro) sisi Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria tumeridhishwa na kazi inayoendelea hapa, huu ni mradi mzuri na wa viwango, tunakupongeza sana sasa ukayafanyie kazi yale masuala madogomadogo tuliyoyaeleza hapa” akasema Makamu Mwenyekiti wa Kamati.
Akaongeza kwa kusema miradi kama hii inayosogeza huduma za kisheria karibu na wananchi na ambayo ndiyo dhamira ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kisheria bila usumbufu wowote.
“Miradi kama hii ambayo ni ya mfano inatupatia sisi wajumbe nguvu ya Kwenda kuizungumzia kwenye kamati zetu na kuziombea fedha ili iweze kuenea nchi nzima”. Akaseme Mhe Kyombo.
Akijibu hoja za wabunge hao ikiwamo ya mapendekezo ya mkandarasi kuongezewa muda kwa kile walichosema mradi upo nyuma kwa miezi miwili Waziri alikuwa na haya ya kusema.
“ Waheshimiwa wabunge niwashukuru sana kwa kuutembelea mradi huu na kwa ushauri mlioutoa kuhusu suala la kumuongezea muda mkandarasi nieleza wazi kabisa, Serikali haikusudii na wala haitamuongezea muda, mkandarasi afanya analoweza kufanya aukamilishe mradi huu kulingana na makubalianao ambapo ni mwezi Octoba Mwaka huu.” Akasisitiza Waziri na kuongeza.
Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa mkandarasi na mshauri mwelekezi wakati wowote watakapokuwa wana tatizo na ikibidi hata kubadili mfumo wa malipo.
Akatahadharia kwa kusema endepo mkandarasi hata kamilisha mradi huo kwa wakati basi itampasa kuilipa serikali kama taratibu zinavyotaka.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kudumu ya Utawala, Katiba na Sheria ilikuwa mkoani Mwanza ambapo pamoja na kuutembelea mradi wa Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali pia wametembelea Jengo Jumuishi la Utoaji haki la Mahakama ya Tanzania.
Kabla kutembelea miradi hiyo walimtembelea Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe Kigoma Malima ambapo walipokea taarifa ya mkoa.
Kamati hiyo ya Bunge kabla ya kufika Mkaoni Mwanza, walikuwa Mkoa wa Shinyanga na Tabora.
Mwisho
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano