Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali
KAMATI ZA KISHERIA ZA MIKOA NA WILAYA KUENDESHA KLINIKI YA KISHERIA
service image

Kamati za Kisheria zilizoko kwenye Mikoa na Wilaya zitakuwa zikiendesha Kliniki ya Kisheria kwa lengo la kutatua kero mbalimbali za kisheria kwa wananchi katika maeneo yao, hayo yamesemwa wakati wa kikao cha Wadau wa Kliniki ya Kisheria ngazi ya Taifa kilichofanyika tarehe 20 Agosti, 2024 katika ukumbi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma. 

Kikao hicho cha Wadau wa Kliniki ya Kisheria kimewakutanisha wadau wa sheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambao ndio waratibu wakuu wa Kliniki ya Kisheria, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Ardhi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Tume ya Utumishi wa Walimu, Chama cha Mawakili wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Taasisi ya Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka. 

Akizungumza kwenye kikao hicho Mkurugenzi Msaidizi Uratibu wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Ipyana Mlilo amesema lengo kuu la kikao hicho ni kujadili namna ya uendeshaji wa Kliniki ya Kisheria katika ngazi za Mikoa na Wilaya, ambapo ameeleza kuwa Kliniki hizo zitakuwa zikiendeshwa na Kamati za Kisheria za Mikoa na Wilaya ili kuweza kuwafikia Wananchi wengi zaidi. 

“Malengo yetu makubwa ni kuhakikisha kuwa shughuli hizi za Kliniki ya Kisheria zinaendeshwa na Kamati za Kisheria katika ngazi za Miko ana Wilaya, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na wadau waliohudhuria kikao hiki tutakuwa na jukumu la kutoa elimu na kuwajengea uwezo wajumbe wa kamati hizo ili waweze kwenda kutatua kero mbalimbali za Kisheria kwa Wananchi”. 

Aidha Mkurugenzi Msaidizi wa Uratibu ameendelea kusema kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itafanya kazi kwa ukaribu na kamati hizo ili kuhakikisha kuwa Kliniki hizo za Kisheria zinawasaidia Wananchi, pia ameeleza kuwa Ofisi hiyo inaanda utaratibu maalumu wa kuziwezesha kamati hizo kutuma ripoti kuhusu namna zoezi la Kliniki ya Kisheria lilivyofanyika katika ngazi ya Mikoa na Wilaya.

Kwa upande wake Afisa Sheria Mwandamizi kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI Bi. Antelma Mtemahanji, ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria kwa kuandaa kikoa hicho kwa wadau wa Kliniki ya Kisheria huku akitilia mkazo suala la kuwajengea uwezo wajumbe wa Kamati za Ushauri wa Kisheria za Mikoa na Wilaya ili waweze kufanikisha malengo yaliyokusudiwa ya Kliniki hiyo.

 “Naipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuandaa kikao hichi pia nisisitize suala la kuwajengea uwezo wajumbe wa hizi kamati, hili ni jambo muhimu ili kufanikisha malengo ya Kliniki hizi za Kisheria zinazotarajia kuanza katika ngazi za Mikoa na Wilaya hivi karibuni”.

Kikao hicho cha wadau wa Kliniki ya Kisheria ni sehemu ya maandalizi ya kufanyika kwa Kliniki ya Kisheria katika ngazi za Mikoa na Wilaya huku ukiwa ni mwendelezo wa kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi kupitia Kliniki ya Kisheria iliyozinduliwa mwezi Juni 2024 katika viwanja vya Nyerere square Jijini Dodoma

20 Aug, 2024
Maoni