Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali
MAFUNZO YAWEZESHE WATAALAM KUISHAURI SERIKALI VIZURI-DKT. LONGOPA
service image

MAFUNZO  YAWEZESHE WATAALAM KUISHAURI SERIKALI VIZURI-DKT. LONGOPA

Na Mwandishi wetu

Dodoma

13 Septemba 2022

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali   Dkt. Evalisto Longopa amewataka  maafisa wa serikali  wanaoshiriki   mafunzo  ya kuwajengea uwezo   katika  maeneo ya gesi, madini na mafuta  kuitumia vema  fursa hiyo ili  waweze  kuishauri vema  Serikali.

Ameyasema hayo leo  jumanne wakati  akifungua mafunzo  ya siku nne yanayoratibiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  na  kuendeshwa  na   Taasisi ya Kimataifa ya  Afican Legal Support Facitility   ambayo  ipo chini ya Bank ya Maendeleo ya Afrika.

Mafunzo  hayo yanafanyika katika ukumbi wa Igada uliopo katika Hoteli ya Dodoma, Jijini Dodoma  na kuhudhuriwa  na mawakili wa serikali,  wataalamu wa masuala ya  jiolojia,  wahandisi, wachumi na wataalamu wa masuala ya fedha ambapo katika siku ya kwanza watalaamu zaidi ya 30  wanashiriki.

Dkt. Longopa amesema,  mafunzo hayo wamewezekana  baada ya  majadiliano ya muda mrefu na ya kina  baina ya Ofisi ya Mwanasheria  Mkuu wa Serikali   na Bank ya Maendeleo ya Afrika  kuhusu  ufadhili wa program za mafunzo ambazo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inakusudia kutekeleza.

Ni kufuatia majadiliano  hayo AfDB iliweza   kuipatia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  mkopo  nafuu wa   kuendesha program hizo kupitia ALSF.

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amebainisha zaidi kuwa   mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo wataalamu kutoka taasisi za serikali  yamegawanyika katika awamu  tatu

Kwa mujibu wa Dkt. Longopa awamu kwanza na ambayo mafunzo yake yameanza ni kuhusu  masuala ya madini, gesi na mafuta, awamu ya pili  itahusu miradi ya  ubia kati ya  Serikali na  makampuni  binafsi (PPP)na  na awamu ya tatu itahusu madeni ya Nchi.

“Ni  matumaini  yangu  kwamba uwepo wenu leo  na ushiriki wenu utawaongeza maarifa na  kuwaweka katika nafasi nzuri ya kuishauri  serikali, mhuwe huru kujadiliana na kubadilisha uzoefu ili kwa pamoja muweze kuisaidia Serikali katika kufikia maamuzi kwa manufaa ya maendeleo na nchi na watu wake” akasisitiza Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Awali  Mratibu  wa  mafunzo hayo kutoka ALSF  Bi. Manuela Dieng  pamoja na kumshukuru Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa heshima ya kufungua mafunzo hayo amebainisha kwamba ALSF itaendelea kushirikiana na  Tanzania   kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika eneo hilo  la program za kuwajenge uwezo wataalamu katika maeneo mbalimbali.

Washiriki wa  mafunzo   haya pamoja na kufuatiliwa mada zinazowasilishwa pia  wanapata nafasi ya kufanya majadiliano  ya kina miongoni mwao kuhusu  mada hizo pamoja na  kuongezeana maarifa.

13 Sep, 2022
Maoni