MAJALIWA AWATAKA WATUMISHI WA OMMS KUENDELEA KUCHAPA KAZI KWA BIDII

NA MWANDISHI WETU
MTUMBA-Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa leo ( Jumatatu) amefanya ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Majengo ya Wizara na Taasisi za Serikali . Majengo hayo yanajengwa katika Mji wa Serikali eneo la Mtumba Jijini Dodoma
Miongozi mwa Majengo aliyotembelea Waziri Mkuu ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambapo akiwa katika eno hilo alipokelewa na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Kamishna Msaidizi Neema Mwanga, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Evaristo Longopa, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali Rajabu N Mabele pamoja na Wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Akiwa katika eneo la ujenzi la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akiwa ameongoza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe Jenista Mhagama , Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bi. Rosemary Senyamule na viongozi wengine alitoa maagizo mbalimbali kwa Uongozi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali , watumishi wa Ofisi hiyo na Mkandarasi SUMA JKT.
Baadhi ya maagizo aliyoa Waziri Mkuu ni pamoja na kumtaka Mkandarasi SUMA JKT kuongeza kasi ukamilishaji kazi mbalimbali zinazoendelea na ikibidi kuanza sasa kazi usiku na mchana.
Akasema “ Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi ameiamini SUMA JKT kujenga mradi huo, na kwa sababu hiyo yeye ( Waziri Mkuu) hategemei SUMA JKT ikawa ni ya mwisho katika kuukamilisha mradi huo. Meja Jenerali( Mkuu wa JKT) upo hapa ni mategemeo yetu kazi itakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa”
Akasema kukamilika kwa jengo hilo siyo tu kutawafanya watumishi wote wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa katika jengo moja, lakini pia kutarahisisha upatikanaji wa huduma ambazo zote zitapatikana katika jengo hilo. Na akawataka wafanyakazi wa OMMS kuendelea kufanya kazi kwa bidii.
Waziri Mkuu ambaye alionyesha pia kuridhishwa kwake na hatua za maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo ambalo mpaka sasa limefika asilimia 65 alikuwa na haya ya kusema.
“Nimefika hapa kutembelea na kuona maendeleo ya ujenzi wa majengo haya ya serikali na taasisi na kote nilipopita nilichoelewa ni utofauti wa hatua mbalimbali za ujenzi wa majengo haya. Hapa mmefikia asilimia 65 ni jambo nzuri, lakini matarajio yetu ni kwamba jengo hilo litakamlika kwa wakati”.
Akabinisha kwamba lengo la serikali ni kuhakikisha kwamba ifikapo Januari 2024 watumishi wote wa serikali watakuwa wameshahamia katika majengo hayo mapya.
Aidha akasema katika kipindi cha miezi mitatu ya mwisho wa mwaka huu itakuwa ni ukamilishaji wa mahitaji mbalimbali zikiwamo fanicha na mambo mengine ya msingi.
Akizungumzia Zaidi kuhusu ufuatiliaji wa utekelezaji wa mradi huo, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Viongozi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na watumishi wa Ofisi hiyo kuhakikisha wanapita mara kwa mara kukagua kazi zinazoendelea ikiwa ni pamoja na kubaini changamoto zinazojitokeza.
“Viongozi katika ngazi mbalimbali jitahidi kufuatilia na kupita mara kwa mara kuangalia maendeleo ya ukamilishaji wa mradi, hata wafanyakazi mnao wajibu wa kupita na kujionea kazi zinazoendelea kwa maslahi ya Serikali lakini pia wananchi waweze kuona kodi zao zimetumikaje kwa kukamilika kwa majengo haya” akasisitiza Waziri Mkuu.
Akizungumzia kuhusu uagizaji wa baadhi ya vifaa vya ukamilishaji wa majengo hayo kutoka nje kama vile vigae, (tiles) Waziri Mkuu amewashauri watendaji wa Wizara na Taasisi pamoja na Wakandarasi kutumia bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani.
Amesisitiza kuwa haitakuwa jambo jema na si sahihi kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi ili hali kuna viwanda vinavyozalisha bidha hizo hizo hapa nchini.
Akasema kwa kuangiza bidhaa kutoka nje, kwanza, kunaua viwanda vya ndani ambavyo serikali imekuwa ikivipigia debe na kukaribisha wawekezaji, lakini ununuzi huo pia unaodosha fedha za kigeni kwenda nje na kupunguza mzunguko wa fedha.
“Nikiwa pale Wizara ya Ardhi nimeambiwa makontena ya vigae yanasubiriwa kutoka Ujerumani na Uturuki, nikashangaa sana kwa nini waagize Ujerumani na Uturuki wakati tunavyoviwanda vya viage ( Tiles ) kule Mkuranga na Chalinze je viage hivi vya ndani havina ubora mpaka muagize kutoka nje?” Akahoji Waziri Mkuu
Na kuongeza “ lazima tubadirishe muelekeo, hivi wizara zote na taasisi zote zikiagiza bidhaa kutoka nje ni kiasi gani cha fedha za kigeni kinakwenda nje, na je viwanda vya ndani havitoshelezi mahitaji, hili ni lazima tuliangalie upya kama sisi wenyewe hatutanua bidhaa za viwanda vyetu vya ndani ambavyo tunavipigia debe sana je majirani zetu watatuonaje” akahoji tena Waziti Mkuu.
Akasema Serikali imekwisha kuaanda fedha kwaajili ya ukamilishaji wa majengo hayo na kuwataka viongozi kufuatilia.
Awali Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Evaristo Longopa alitoa maelezo mafupi kuhusu maendeleo ya mradi huo.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano
3/7/2023