MENEJIMENTI YA OMMS YARIDHIA MICHORO YA JENGO LA ARUSHA

Na Mwandishi Wetu
Mtumba,Dodoma
Menejimenti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali jana jumatano (Desemba 21,2022) imeridhia michoro ya ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mkoani Arusha.
Kuridhiwa kwa michoro hiyo na Menejimenti kumetokea baada ya Wataalamu kutoka Wakala wa Majengo ( TBA)kuwasilisha nyaraka mbalimbali ikiwamo michoro ya mradi huo pamoja kuelezea hatua kwa hatua za mchakato mzima wa maandalizi ya eneo la ujenzi.
Akielezea mchakato mzima ulivyokuwa na utakavyokuwa katika utekelezaji wa mradi huyo , Mhandisi Juma Dand ambaye ni Kaimu Wakala wa Majengo Mkoa wa Arusha, alibainisha kuwa TBA kama mshauri mwelekezi imezingatia masuala yote ya msingi yakiwamo yanayohusu masuala ya mazingira na matumizi endelevu ya ardhi kwa kukutana na kuwa na vikao na wadau mbalimbali.
Mhandisi Dand akatumia fursa hiyo pia kuushukuru uongozi wa Ofisi ya Mwasheria Mkuu wa Serikali kwa kuendelea kuimaini Taasisi na kuipa kazi ya kuwa mshauri mwelekezi wa mradi Arusha.
Katika maelezo yake kwenye kikao hicho ambacho kilikuwa chini ya Uenyekiti wa Kaimu Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Onorius Njole , Mhandisi Dand alitaja baadhi ya matakwa ambayo yapaswa kuzingatiwa ni pamoja kulinda mazingira ya mto unaopita katika eneo la mradi.
Kwa upande wake Kaimu Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Njole amewashukuru wataalamu hao wa TBA kwa kazi ya maandalizi ya mradi huo pamoja na ufafanuzi walioutoa kutokana na maswali yaliyoulizwa na wajumbe wa kikao.
“Tunawashukuru kwa kuja kwenu na kwa maelezo na ufafanuzi mliotoa, tunaridhia pamoja na michoro mliyotuonyesha lakini pia kuna mapendekezo machache tuliyotoa basi mtaangalia namna gani ya kuyafanyika kazi”. Akasema Bw. Njole.
Kikao hicho cha Menejimenti kilihudhuriwa pia na Maafisa Waandamizi kutoka Divisheni na Vitengo vya OMMS.
Kiwanja cha Mraji wa Jengo la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kina ukubwa wa mita za mraba 2901 na kipo katika barabara ya Arusha- Moshi kati ya Hoteli ya Mount Meru na Pan African Postal Union na umbali mfupi kutoka ilipo Mahakama Kuu.
Jengo la Arusha ambalo ramani yake inafafana na jengo la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali mkoani Mwanza na litakuwa Jengo Jumuishi la Taasisi za Kisheria kama ilivyo Mwanza.
Taasisi za Kisheria zitakazotumia Jengo la Arusha ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu.
WAKATI HUO HUO, leo ( alhamisi) Bodi ya Ununizi ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imepitisha njia ya manunuzi kwaajili ya kumpata Mkandarasi atakayejenga jengo la Arusha.
Bodi hiyo ilikutana chini ya Kaimu Mwenyekiti Bw. Buji Bampebuye imefanya kikao chake katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Ipagala.
Mwisho
22/12/2022