MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI AAPISHWA BUNGENI JIJINI DODOMA
Mhe Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Hamza Johari amekula kiapo cha uaminifu mbele ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson, tarehe 27 Agosti 2024. Mwanasheria Mkuu ameapa kabla ya kuanza kikao cha kwanza cha Mkutano wa kumi na sita (16) wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mhe. Mwanasheria Mkuu wa Serikali amepishwa kwa mujibu wa Ibara ya 59(5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 inayompa Mamlaka ya kuwa mbunge na kuhudhuria vikao vya Bunge. Vilevile mara baada ya uapisho huo Mwanasheria Mkuu wa Serikali alikabidhiwa nyaraka mbalimbali za kumuwezesha kufanya kazi akiwa Bungeni na Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson.
Aidha kuapishwa kiapo cha uaminifu mbele ya Bunge kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kunafuatia uteuzi uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kumteua Bw. Hamza Johari kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mnano tarehe 15 Agosti 2024 na kufuatia na uapisho uliofanyika tarehe 16 Agosti 2024 Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Mhe Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Hamza Johari amechukua nafasi ya Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi ambae ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, ambapo kabla ya kuteuliwa kwake kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Hamza Johari alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCCA).