SAMIA ATIMIZA AHADI YAKE KWA MAWAKILI WA SERIKALI

Na Mwandishi Maalum
Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa komputa mpakato 150 kwaajili ya mawakili wa serikali ikiwa ni ahadi yake aliyoitoa wakati wa Mkutano Mkuu wa Mawakili wa Serikali uliofanyika Mwezi Septemba 2022.
Vifaa hivyo vya Tehama, vimekabidhiwa jana jumatano kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe Dkt Moses Mpogole Kusiluka aliyekabidhi kwa niaba ya Mhe. Rais katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu na kushuhudiwa na Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu na Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende.
Akizungumza katika hafla ya hiyo ya makabidhiano, Katibu Mkuu Kiongozi amesema, ni matumaini ya Mhe. Rais kuwa, vifaa hivyo vya tehama vitaboresha na kuongeza ufanisi wa mawakili wa serikali katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Tumekutana katika hafla hii fupi lakini muhimu sana. Mhe Rais alitoa maelekezo tukutane ili nikukabidhi vifaa hivi vya Tehama ambayo Mhe Rais aliridhia wakati wa Mkutano Mkuu wa Mawakili wa Serikali uliofanyika mwezi septemba 2022 hapa Dodoma”. Akaeleza Katibu Mkuu Kiongozi
Na kuongeza “ Ni matarajio ya Mhe. Rais kuwa vitendea kazi hivi vitatumika kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao mawakili wa serikali na hasa kwa kuzingatia umuhimu wa matumizi ya tehama katika tasnia ya sheria”.
Katibu Mkuu kiongozi Kusiluka akaeleza zaidi kwa kusema “ Sote tunafahamu Mhe. Rais ametoa kipaumbele katika kuboresha mifumo ya haki jinai na haki kwa ujumla, hivyo basi juhudi za Rais na serikali kupitia msaada huu ni kuona ufanisi wa mawakili wa serikali nao unaongezeka”.
Vile vile Mhe. Kusiluka amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwasaidia Mawakili wa Serikali kadri itakavyowezekana hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali imejikita katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati, miradi ambayo inahitaji wataalamu wabobevu katika kila eneo wakiwamo Mawakili wa Serikali.
“ Serikali inathamini mchango wa mawakili wa serikali, ni matumaini ya Rais na ya kwangu kwamba, nyinyi viongozi wa Taasisi mtaendelea kusaidia na kuhamasisha wataalamu wenu kuisaidia serikali katika utekelezaji wa miradi hii ya kimkakati” akasisitiza Katibu Mkuu Kiongozi.
Kwa upande wake akizungumza baaada ya kukabidhiwa vifaa hivyo vya Tehama, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi amesema Komputa mpakato hizo zitaleta heshima kubwa kwa mawakili wa serikali.
“Kwa niaba ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, nitoe shukrani zangu za dhati kabisa kwa Mhe. Rais kwa kuridhia na kutupatia vifaa hivi vya tehama ametuangalia kwa jicho la umama na kwa kweli ni upendo wake wa dhati” akasema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Akasema , wakati wa mkutano Mkuu wa Mawakili wa Serikali uliofanyika Septemba 29 mwaka jana , Mkutano ambao Mhe. Rais alikuwa mgeni rasmi na pia akazindua Chama cha Mawakili wa Serikali alibainisha changamoto mbalimbali zikiwamo za uhaba wa vitenda kazi kwa maana ya Vifaa vya Tehama kwa mawakili wa Serikali
“Katika Mkutano ule tulielezea changamoto mbalimbali zikiwamo za miundombinu, upungufu wa watumishi ,lakini tukaelezea hili la vitendea kazi kwa maana ya vifaa vya tehema ili kwenda sambamba na maboresho yanayoendelea katika Tasnia ya Sheria”. Akasema Mwanasheria Mkuu
“Hata katika majadiliano ya migogoro baina ya Serikali na wadau wetu vikao vingi vinafanyika kwa njia ya Tehema jambo ambalo mawakili wetu wapo nyuma kutokana nakutokuwa na na vitenda kazi vya kisasa. Vifaa hivi vitaleta heshima kubwa kwa mawakili wetu wa Serikali wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao” akasisitiza Mhe. Feleshi.
Aidha Mhe Feleshi akasema, vifaa hivyo vya Tehama si kwamba vinahitajika kwa Mawakili wa Serikali peke yao bali hata kwa Divisheni na Vitengo wezeshi akitolewa mfano wa Kurugenzi ya Utawala na Raslimali Watu , Kurugenzi ya Mipango na Masijala
“ Mhe Katibu Mkuu Kiongozi, tunafahamu mchakato huu umegharimu fedha na muda wa Mhe Rais na Serikali, sisi sote hapa ni wateule wa Rais na ukisha kuwa mteule wa Rais huna mambo yako, tunafuatilia na kusikiliza shughuli za Mhe Rais niahidi kwamba tutatumia vifaa hivi ili kwa pamoja na Serikali tuweze kuleta nafuu kwa watanzania” Amesisitza Mhe. Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mwisho
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano
22/03/2023