TAASISI ZA KISHERIA ZIACHWE ZIJIPANGIE MAMBO YAO- AG FELESHI

Na Mwandishi Maalum
28/11/2022
MWANZA
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi amesema, ifikie mahali sasa kwa Taasisi za Kisheria nchini ziachwe zijipangie mambo yao kwa namna zinavyoona badala ya kupangiwa.
Amesema ni kwa kujipangia mambo yao na mipango yao ndipo Taasisi hizo zitakayoweza kwa ukamilifu na kwa tija kuisaidia Serikali kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
Kwa sababu hiyo Dkt Feleshi, amezihimiza taasisi hizo ambazo ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali zianze zenyewe kujisahihisha na kutorudia makosa ya nyuma ya kupangiwa mambo yanayohusu majukumu yao.
“ Kama binadamu tunaishi kwa kujisahihisha , na kujisahihisha si vibaya kwa sababu ni kwa kujisahihisha unakuwa na hamu ya kwenda mbali sana. Kwa hiyo sisi kama Taasisi za kisheria tunapaswa kujisahihisha ili tusirudie makosa ya nyuma ya kutojipangia mipango yetu tunavyotaka wenyewe na kuimilika mipango hiyo”. Amesisitiza AG Feleshi
Alikuwa akifungua kikao Jumuishi cha Menejimenti kutoka Taasisi hizo tatu, kikao ambacho, pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kimehudhuriwa pia na Mkurugenzi Mkuu Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Bw. Sylvesta Mwakitalu na Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Bonifance Luhende.
Kikao hicho kimepokea na kujadili taarifa ya maendeleo ya Muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali . Kikao kimefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
.
Pamoja na kusisitiza umuhimu wa taasisi hizo tatu kujisahihisha na kutorejea makosa ya nyuma, amesisitiza pia haja na umuhimu kwa taasisi hizo tatu kuwa na uwajibikiaji wa pamoja bila kuathiri nafasi au majukumu ya kila Taasisi .
“Uwajibikaji wa pamoja utahakikisha Taasisi hizi zote zinafanikiwa kwa pamoja katika utekelezaji wa majukumu yao, tukiwa na uwajibikaji wa pamoja na ushirikiano wa pamoja tutakuwa na sauti ya Pamoja na tutakuwa na nguvu kubwa ya kuisaidia serikali ” akabainisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka.
Kwa upande wake , Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ( DPP) Bw. Sylvesta Mwakitalu yeye amesema, Taasisi hizo tatu ni taasisi muhimu sana katika kuhakikisha haki, amani na maendeleo ya taifa la Tanzania.
“ Wote tunafahamu umuhimu wa Ofisi hizi Tatu kwa maendeleo na ustawi wa nchi yetu. Kama Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ikilegea, ikiwa watumishi wake hawatatimiza majukumu yao kwa makusudi au kwa bahati mbaya au kwa uzembe mnajua madhara yake ni nini kwa Serikali” akasema DPP Mwakitalu na kuongeza
“Kama Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ikilegalega katika utekelezaji wa majukumu yake sote tunajua namna gani maamuzi yanayotolewa na mahakama yatakavyowaumiza watanzania.
Akaoongeza “Ofisi ya Mataifa ya Mashtaka tusipofanya kazi yetu ipasavyo hakutakuwa na amani, biashara hazitafanyika, uchumi hautakua lakini pia nchi haitakalika.
Kwa sababu hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka amesema anafurahishwa sana na namna ambavyo Taasisi hizo tatu zimeanza kuwa na mashirikiano na mahusiano ya karibu katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Hiki ni kikao cha kihistoria, ninaona mwanga mpya tukitumie kikao hiki kujadiliana namna bora ya utekelezaji wa majukumu yetu kikoa ambacho kitatupa mwelekeo wenye tija kwa taasisi zetu na watumishi wake kwa ujumla
Naye Wakii Mkuu wa Serikali Dkt Bonifance Luhende naye akizungumzia kuhusu kikao jumuishi cha Menejimeti za Taasisi hizo tatu, amesema, kikao hicho kinafanyika wakati muafaka na kitatoa fursa ya kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili Taasisi hizo.
“Jukwaa hili linatupa fursa ya kujadili na kutathimini hali ilivyo sasa katika taasisi zetu, hali ya utekelezaji wa majukumu yetu, hali ya watumishi wetu je hali zao zinaendana na majukumu makubwa na mazito wanayoyatekeleza, jukwa hili litufanya tuwe na sauti moja na Kwenda kama kundi moja”. Amesitiza Dkt. Luhe
Pamoja na Viongozi Wakuu wa Taasisi hizo, viongozi wengine waliohudhuria kikao hicho ni Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Evaristo Longopa, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Bi. Sara Mwaipopo na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Joseph Pande, Wakurugenzi, Wakurugenzi wasaidizi, Wakurugenzi wa Mipango, Wakuu wa Vitengo vya Manunuzi na Wataalamu wengine kutoka Taasisi hizo tatu.
Wakati huo huo Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro kesho ( Jumanne) ataweka Jiwe la Msingi la Jengo la Kituo Jumuishi cha Taasisi za Kisheria.
Jengo hilo linajengwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika eneo la Buswero Mkoani Mwanza na litahudumia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na RITA.