Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali
Tanzania yaombwa kuridhia baadhi ya Itifaki za Mkataba wa Kimataifa kuhusu masuala ya Nyukilia
service image

Na Mwandishi Maalum

Dodoma

Tanzania  imeombwa kuridhia baadhi ya  itifaki za mabadiliko ya Mkataba wa Kimataifa wa  Ulinzi wa Nyezo za Nyukilia (Convention on the Physical Protection of Nuclear Material).

Ombi hilo limetolewa  siku ya ,  jumatano  na  Bw. Richard Sseggane kutoka  Shirika la  Kimataifa la Nguvu za  Atomu Duniani ( IAEA) wakati ujumbe kutoka IAEA  ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania Profesa Lazaro Busagal ulipoitembelea  Ofisi ya  Mwanasheria Mkuu wa Serikali jijini Dodoma  na  kufanya  mazungumzo na  Mwandishi Mkuu wa Sheria    Bw. Onorius Njole.

Bw. Sseggane amebainisha kwa kueleza kwamba,  ingawa Tanzania imeridhia Mkataba huo, (The Convention on the Physical Protection of Nuclear Material) lakini bado haijaridhia  baadhi ya  itifaki za mabadiliko ya mkataba huo,  hivyo basi,  wanaiomba  Tanzania, kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  ambayo ni mdau mkubwa katika  mchakato wa uridhiaji wa mikataba ya  kimataifa kusaidia.

“Tunaiomba Ofisi ya  Mwanasheria Mkuu wa Serikali  iendelee kushirikiana na Tume ya Nguvu za  Atomu Tanzania na Wizara husika katika  kufanikisha  kuridhiwa kwa  Itifaki zilizobakia”, akasihi Bw. Richard Sseggane kutoka IAEA.

Ujumbe huo  pamoja na  kuzungumzia kuhusu  Mkataba  huo pia walizungumzia mkataba mwingine  wa kimataifa wa Utokomezaji wa Vitendo vya Ugaidi wa Nyukilia. “the International Convetion for Suppression of Acts of Nuclear Terrorism".

Aidha   Ujumbe huo   umeishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuendelea kuwa  mdau muhimu  katika masuala ya nguvu za atomu hususani katika  eneo la maboresho ya sheria.

Kwa upande wake,  Mwandishi Mkuu wa Sheria  Bw. Onorius Njole aliyekuwa mwenyeji wa Ujumbe huo kwa  niaba ya  Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ameuhakikisha Ujumbe huo kwamba, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  itakuwa tayari kutoa ushirikiano wowote utakaohitajika katika eneo  hilo.

Aidha   Mwandishi Mkuu wa Sheria  ameushukuru  Ujumbe huo  kwa  kutoa maelezo ya kina  kuhusu Mikataba hiyo ya Kimataifa  lakini pia kwa  kuitembelea Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  na kutambua  nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  katika  masuala  yote  yanayohusu  mikataba ya  kimataifa.

Bw. Onorius  Njole    alitumia fursa hiyo kuelezea majukumu mbalimbali ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yakiwamo  ya mapitio ya sheria mbalimbali  za kitaifa na kimataifa  pamoja na na mchakato wa kuzitafsri sheria hizo katika lugha ya Kiswahili.

Mwisho.

Imeandaliwa  na Maura Mwingira

Mkuu wa   Kitengo cha Mawasiliano

Ofisi ya Mwanasheria  Mkuu wa Serikali

26 Oct, 2022
Maoni