TLS WADAU MUHIMU KATIKA KUSIMAMIA WA UTAWALA WA SHERIA –AG FELESHI

TLS WADAU MUHIMU KATIKA KUSIMAMIA WA UTAWALA WA SHERIA –AG FELESHI
Na Mwandishi Maalum
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Dodoma
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dk. Eliezer Feleshi ( AG) ameutaka uongozi mpya wa Chama cha Mawakili wa Kujitegemea Tanzania Bara ( TLS) kuwa na mifumo ya kiutendaji ambayo pamoja na mambo mengine itasaidia na kurahisisha ushirikiano kati ya Chama hicho na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Ametoa rai hiyo mwishoni mwa wiki jijini Dodoma, wakati Ujumbe wa Baraza la Uongozi la TLS ukiongozwa na Rais wa Chama hicho Profesa Edward Hosea ulipomtembelea Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa lengo la kujitambulisha na kubadilishana naye mawazo kufuatia uchaguzi wa chama hicho uliokamilika hivi karibuni.
Katika mazungumzo hayo, uongozi wa TLS uliwasilisha hoja mbalimbali ambazo wamemwomba Mhe. AG kuwasaidia kuzifutailia.
Baadhi ya hoja hizo ni pamoja na ombi la kurejeshwa sehemu ya malipo ya wanachama wao zinazolipwa Mahakamani ombi ambalo wamesema kwa msaada wa AG Feleshi linaendelea vizuri.
“Niwapongeze kwa kuchaguliwa kwenu, wanachama wenu wamewaamini, TLS ni mdau muhimu katika tasnia ya sheria na hususani katika utawala wa sheria. Hivyo niwaombe muwe na mifumo mizuri ya kuitendaji ambayo pamoja na mambo mengine itawezesha kubaini mawakili wabobezi katika maeneo mbalimbali ambao Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itapenda kuwatumia pale itakapohitaji kufanya hivyo” amesisitiza AG Feleshi.
Kuhusu hoja ambazo TLS wameomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali kusaidia kuzifutalia. AG Feleshi ameahidi kuendelea kuwasaidia kufuatilia kwa baadhi ya hoja ambazo zimo ndani ya mamlaka yake, ikiwamo ya kiwanja ahadi ambayo aliitoa mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Aidha kwa hoja ambazo zipo nje ya mamlaka yake zikiwamo za mabadiliko ya kisheria ili pamoja na mambo mengine, kuongeza muda wa kufanya uchaguzi wa viongozi wa TLS, ameutaka uongozi huo kufuatilia katika Taasisi husika ikiwamo Wizara ya Katiba na Sheria.
AG Feleshi ameahidi utayari wa Ofisi yake wa kushirikiana na TLS katika kutekeleza majukumu ya kisheria kwa maslahi mapana ya umma wa watanzania na akawataka TLS kuwa mabalozi na jicho katika utekelezaji wa majukumu hayo.
Kwa upande wao Uongozi TLS pamoja na mambo mengine umetumia nafasi hiyo kumpongeza kwa mara nyingine Mhe. Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuteuliwa kwake kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Na kumshukuru kwa namna ambavyo amekuwa tayari kushirikiana na TLS ikiwa ni pamoja na kusukuma hoja zao mbalimbali.