TUME YA RAIS YA KUBORESHA HAKI JINAI YAKUTANA NA WADAU MKOANI MWANZA

Na Mwandishi wetu
Wajumbe wa Tume ya Rais ya kuangalia namna ya kuboresha Taasisi za Haki jinai wanaendelea na zoezi la kutembelea Taasisi mbalimbali pamoja na kukusanya maoni kutoka kwa viongozi wa Taasisi hizo na Makundi mbalimbali ya jamii.
Katika kutekeleza majukumu hayo, wajumbe hao wamegawanyika katika makundi tofauti.
Kuanzia siku ya jumatatu Marchi 6 ,2023) Mwenyekiti wa Tume hiyo Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu Mohammed Othman Chande akiwa amefuatana na baadhi ya wajumbe wa Tume Mhe. Jaji Dkt .Eliezer Feleshi Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu Bw. Said Mwema wapo Mkoani Mwanza.
Wakiwa Mkoani humo Wajumbe hao pamoja na kukutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wao Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima wamepata fursa ya kutembelea Taasisi mbalimbali za Haki jinai zikiwamo vituo vya Polisi kikiwamo Kituo Kikuu cha Polisi Mwanza na Gereza Kuu la Butimba.
Wakiwa katika Taasisi hizo, Wajumbe hao walipata taarifa kutoka kwa viongozi wanaosimamia taasisi hizo ( Magereza na Polisi) na pia waliweza kuzungumza na wafungwa.
Pia timu hiyo ilipata fursa ya kuwa na kikao na wakuu wa Taasisi za Haki jinai mkoani Mwanza, wakiwamo Polisi , Magereza, Takukuru, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka , Uhamiaji, na Taasisi inayohusika na Madawa ya kulevya.
Aidha wajume wa Tume hiyo pia walipata fursa ya kuwa na mikutano ya hadhara ambapo pamoja na kuelezea majukumu ya Tume hiyo. Mwanasheria Mkuu wa Serikali alielezea kwa kina na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu suala zima na maana ya Haki Jinai na mnyororo mzima wa haki jinai.
Baada ya Maelezo hayo ya kina Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika mkutano wake na wananchi katika wilaya ya Misungwi alitoa nafasi kwa wananchi kuelezea kero zao na hata kuuliza maswali katika eneo hilo la uboreshaji wa haki jinai nchini
Itakumbukwa kwamba Mwezi jaruani Mwaka huu, Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliunda Tume ya Rais ya kuangalia namna ya kuboresha Taasisi za haki Jinai nchini na akaipa Tume kukamilisha kazi ifikapo mwezi April mwaka huu.
Tume hiyo inaongozwa na Mhe. Mohammed Othman Chande ambaye ni mwenyekiti, Balozi Omben Sefue Makamu Mwenyekiti na wajumbe wakiwa ni Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Edward Hosea, Said Ally Mwema, Balozi Ernest Magu, Dkt. Laurean Ndumbaro na Bw. Omary Issa.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano
7/3/2023