Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali
UKIPEWA OFISI CHAPA KAZI USISUBIRI KUPANDISHWA CHEO -AG FELESHI
service image

Na Mwandishi Maalum

Dodoma

Mwanasheria Mkuu wa Serikali   Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi  amekuwa na kikao kazi  na Watumishi  wa Kada zote  wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  .

Katika Kikao Kazi hicho na ambacho ni cha  Kwanza cha aina yake kimefanyika  siku ya Alhamisi katika ukumbi wa mikutano  ulipo katika  Jengo la Mkapa  Jijini   Dodoma.

Mhe MMS ametumia kikao kazi hicho   kufahamiana na watumishi,  kuwapongeza  kwa utekelezaji mzuri  wa majukumu yao ya kila siku na vilevile  kukumbushana  masuala mbalimbali.

 Amewaeleza   watumishi hao kuwa,   kutokana na mazingira ya utekelezaji wa majukumu , imekuwa si rahisi sana kukutana  wote kwa pamoja,  kusalimiana na kuzungumza,  “wengine wapo  Ipagala wengine wapo Mtumba,  kwa hiyo kunachangamoto kidogo  ya ufinyu wa mahali  pa kukutana  ninaomba jengo  jipya likamilike mapema”akaeleza MMS Feleshi.

Akaongeza  kwa kusema zimebakia siku chache kabla  hajatimiza mwaka mmoja  tangu alipoteuliwa na Mhe. Rais kuwa  Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  na  kama  wanafamilia  ameona kunahaja na umuhimu wa kuwa na  kikao kazi hicho na watumishi wote.

“Kwanza niwapongeze kwa kazi nzuri , pamoja na changamoto mbalimbali mmekuwa  mkitekeleza majukumu  yenu vizuri ingawa katika utekelezaji wa majukumu hayo kuna maumivu mnapitia lakini kazi  zinaendelea niwapongeze katika hili “ akasitiza Mhe. MMS ana kupigiwa makofi na watumishi.

Baadhi ya  masuala ambayo  MMS amesisitiza katika   kikao kazi hicho ni  umuhimu   kuendelea kuweka  mazingira ya kila mtumishi  katika Divisheni na kitengo ajue  kinachoendelea katika  Divisheni au Kitengo kingine. Kwa kile alichosena Ofisi ya  Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndiyo nyumbani kwa watumishi wenyewe,  kwa serikali na wadau wengine.

Na akawataka watumishi kuishi kama familia moja,  kujithamini , kujitambua, na kuvumiliana.

Akawakumbusha  Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo kujijengea utamaduni  wa kuwafahamu  watumishi waliochini yao na kwa kufanya hivyo wataweza kutambua uwezo wa  kila mmoja wao lakini pia kufahamu changamoto  mbalimbali wanazopitia iwe za kikazi au za kifamilia.

Mhe. Feleshi amewahimiza pia watumisishi kulitumia sanduku la maoni kutoa  madukuduku  yao au kwenda kwa watu wanaowamini. Na kusisitiza  kwa mara nyingine hapendi majungu.

“Mtu asijione  hana furaha, hii Ofisi  ni ya kila mtu hivyo kila mmoja wetu ajione ana umiliki wa Ofisi na  tufanye kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma” Amesisitiza Mhe. AG.

 “ Ukishapewa Ofisi fanya kazi haki zako za kiutumishi zipo tu, kila mmoja wetu ajiamini katika eneo lake la kazi kwa kuchapa kazi hata kama upandishwaji wa daraja lako unachelewa wewe chapa kazi kwani haki zako za kiutumishi  zipo  palepale” amesema

Kuhusu watumishi wanaokaimu  Divisheni au Vitengo amewataka kujiamini katika nafasi hizo badala  ya kukaa nusu nusu.

Vile vile amewakumbusha na kuwahimizi watumishi  wote matumizi ya  E-  Office katika utekelezaji wa majukumu na kwamba dunia hivi sasa  inaachana na kukimbizana na  majalada.

Pamoja  na matumizi ya TEHAMA amesisitiza kwa kila Afisa anayekwenda safari za  kikazi  kuandika taarifa  ya safari hiyo mara anaporejea Ofisi.

Sambamba na hilo amerejea tena umuhimu wa watumishi kujiendeleza kwa faida yao lakini  pia amesisitiza maendeleo ya kitaaluma yaendane na maendeleo  katika ngazi ya familia na katika hili  amesisitiza haja na muhimu  kukamilishwa kwa  sera ya mafunzo na kuimarishwa kwa  Sheria Saccos pamoja na kuongeza idadi ya wanachama.

Ametilia  umuhimu  wa watumishi wote kujifunza namna bora ya kuandika  Wasifu wao ( CV)  kwa kile alichosema wengi hawajui kuandika wasifu zao na wakiacha mambo ya msingi yanayoiongezea uzito  wasifu huo. Pia  wawe na utamaduni wa kuboresha wasifu  zao kila mara.

Kuhusu  Mkutano Mkuu wa Mawakili utakaofanyika mwishoni mwa Mwezi wa  Septemba, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewataka watumishi wote kushiriki kikamilifu  katika mkutano huo, mkutano ambao  mgeni Rasmi atakuwa  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akatumia  pia  fursa hiyo kuipongeza Kamati ya maandalizi ya Mkutano huo.

Mhe. Feleshi ametaka kufanyika  mkutano wa wafanyakazi wote angalau  mara mbili  kwa mwaka.

Katika hatua nyingine amemuagiza Mkurugenzi wa Mipango kuanza  mapema maandali ya bajeti ya mwaka wa fesha 2023/24.

Awali akimkaribisha Mwanasheria Mkuu kuongeza na  watumishi, Kaimu Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Francis Kayichile alisema watumishi waliohudhuria kikao hicho walikuwa zaidi ya 80  kati ya watumishi  wote. Na kwamba wengine hawakuhudhuria kutoka  kuwa nje ya  Ofisi kwa shughuli za kikazi.

mwisho

 

 

08 Sep, 2022
Maoni