WANASHERIA EACOP WAMTEMBELEA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI

WANASHERIA EACOP WAMTEMBELEA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amekutana na kufanya mazungumzo na Bw. Stanley Mabiti, Meneja Sheria wa Mradi wa Bomba la Mafuta la Afrika Mashariki ( EACOP).
Mazungumzo kati ya Mhe. Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Bw. Mabiti yamefanyika jana tarehe 12/12/2022 katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jijini Dar es Salaam. Mazungumzo yalihudhuriwa pia na Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniface Nalija Luhende.
Bw. Mabiti aliambatana na Mshauri wa Sheria wa mradi huo (EACOP) Bw. Yohana Mganga ambao waliomba kuonana na Mhe. Jaji Dkt. Feleshi kwa madhumuni ya kufahamiana naye na kumfahamisha masuala mbalimbali yanayohusiana na maendeleo ya mradi huo wa EACOP.
Meneja Sheria wa EACOP Bw. Mabiti pia aliwasilisha hoja juu ya haja ya kufanyika warsha ya kuzijengea uelewa wa pamoja Taasisi zote za Serikali zinazohusika katika utekelezaji wa Mkataba wa Nchi Hodhi za Mradi wa Bomba hilo la Mafuta.
Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Feleshi aliwashukuru wataalamu hao kwa kumtebelea na kubadilishana naye mawazo kuhusu utekelezaji wa mradi huo ambao ameutaja kuwa wenye Tija kwa Taifa.
Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashari ni Mradi Shirikishi kati ya Tanzania na Uganda ambapo bomba hilo linajengwa kuanzia Kabale-Hoima Nchini Uganda hadi Peninsula ya Chongolani Mkoani Tanga Nchini Tanzania.
Mradi huo una urefu wa jumla ya kilomita 1443 ambapo kati ya hizo, kilomita 296 zipo nchini Uganda na kilomita 1147 zipo nchini Tanzania.
Lengo la Mradi huu ni kuwezesha mafuta yatakayozalishwa nchini Uganda kusambazwa katika soko la ndani na sehemu itakayosalia kuuzwa nje kwenye soko la Kimataifa kupitia bomba hilo.
Mwisho.
Maura Mwingira
Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Serikalini
13/12/2022