WATUMISHI OMMS WAPATIWA SEMINA KUHUSU AFYA YA AKILI SEHEMU YA KAZI

Na Mwandishi wetu
Mtumba-Katika miaka ya hivi karibuni pamekuwapo na taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vinavyoelezea ongezeko la changamoto zinatokana na afya ya akili au msongo wa Mawazo.
Matatizo hayo mawili yamekuwa yakiwakumba watu wa kada tofauti tofauti wakiwamo wafanyakazi.
Ingawa hakuna twakimu sahihi lakini hakuna ubishi kwamba tatizo la au changamoto ya afya ya akili na msongo wa Mawazo ni kati ya magonjwa ambayo si ya kuambukiza lakini yanayochangia kwa kiasi kikubwa maendeleo na utendaji kazi kwa idadi kubwa ya watu.
Katika kutambua uwepo wa changamoto hiyo, Divisheni ya Uratibu na Huduma za Ushauri wa Kisheria(DCAS) Alhamisi Septemba 22,2023 iliandaa mafunzo ya siku moja kuhusu Afya ya Akili kwa Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Mafunzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa Mikutano Mtumba Jijini Dodoma
Semina au mafunzo hayo kuhusu suala la afya ya akili mahali pa kazi yalitolewa na Dkt. Garvin Nathaniel Kweka kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambaye pia ni Daktari mbomezi wa ya magonjwa ya Figo.
Akimkaribisha mtalaam huyo Mkurugenzi wa Divisheni ya Uratibu na Huduma za Ushauri wa Kisheria Dkt. Gift Kweka, alisema, Divisheni yake iliamua kuratibu semina hiyo hasa kwa kuzingatia uzito na aina ya majukumu yanayotekelezwa na watumishi wa OMMS majukumu ambayo kwayo ndani yake yana stress nyingi.
“tumeona kuna haja na umuhimu tukapata semina au mafunzo haya kuhusu afya ya akili ili yatusaidie sisi kama watumishi wa OMMS kuweza kuweka uwiano mzuri katika utekelezaji wa majukumu yetu na namna bora ya kukabiliana na stress zinazotokana na majukumu hayo ili kwa ujumla itusaidie kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi na tija lakini kama watu binafsi tuwe na afya bora ya akili”. Akasema Mkurugenzi Kweka.
Semina au mafunzo hayo yalihudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Divisheni ya Utawala na Raslimali Watu Bw. Silas Marwa, na Watumishi kutoka Divisheni nyingine ikiwamo Divisheni iliyoratibu mafunzo hayo (DCAS)